Habari
WAZIRI SILAA AZIPONGEZA TAASISI ZA MAWASILIANO KWA MSHIKAMANO WA KUKUZA MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA KUHUDUMIA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa amezipongeza taasisi za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) kwa mshikamano unaoonesha uthabiti wa Serikali katika kuhakikisha Sekta ya Posta na Mawasiliano kwa ujumla inaendelea kuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akihutubia wakati wa hafla fupi ya makabidhiano, ambapo UCSAF imekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa TPC vyenye thamani ya shilingi milioni 288 leo Agosti 22, 2025 jijini Dar es Salaam Waziri Silaa ameitaka TPC kuhakikisha inatumia vifaa hivyo kwa ufanisi ili kuongeza thamani ya huduma na kuimarisha uaminifu wa wananchi.
“Kwa mshikamano huu, tutaijenga Tanzania yenye huduma za kisasa za posta zinazokidhi viwango vya kimataifa, na kumwezesha kila mmoja kunufaika na fursa hizi za kidijitali”, amesisitiza Waziri Silaa.
Aliongeza kuwa, “Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka msimamo wa wazi kwamba huduma za msingi kama posta, mawasiliano ya simu, intaneti na huduma za kifedha za kidijitali si anasa tena, bali ni haki ya kila Mtanzania”.
Alifafanua kuwa mashirika ya posta duniani, kupitia Umoja wa Posta Duniani (UPU) na Umoja wa Posta Afrika (PAPU), yameweka vipaumbele vya kubadilisha utoaji wa huduma kutoka mfumo wa zamani kwenda mfumo wa kisasa wa kidijitali ili kuwezesha utoaji wa huduma bora, za haraka na salama katika maeneo yote ya miji na vijiji.
“Vifaa hivi si tu kwamba vitaboresha kasi ya usambazaji wa barua na vifurushi, bali vitafungua pia milango ya huduma mpya kama biashara mtandao, malipo ya kidijitali na huduma za Serikali mtandao. Huu ndio mwelekeo wa dunia, na Tanzania haiwezi kubaki nyuma,” alisema Waziri Silaa.
Katika hatua nyingine ameitaka UCSAF kuendelea kusimamia miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi na kuhakikisha kila uwekezaji una matokeo chanya na yanayopimika kwa usimamizi wa Wizara anayoiongoza.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Mkapa, ameipongeza UCSAF kwa kukabidhi vifaa hivyo kama kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha matumizi ya teknolojia katika huduma za mawasiliano na posta yanawafikia wananchi wote, popote walipo.
“Tukio hili ni ishara ya matokeo ya Serikali katika kuhakikisha dhana ya matumizi ya teknolojia katika huduma za mawasiliano na posta zinawafikia wananchi maeneo yote walipo,” alisema Mkapa.