Habari
WAZIRI SILAA ATAKA USIMAMIZI BORA WA MFUMO WA USAFIRISHAJI WA SWIFPACK

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) ameliagiza Shirika la Posta Tanzania kuhakikisha mfumo wa Swifpack unatunzwa na kuimarishwa, akisema kwamba huduma hii ni ya kisasa na ya kimkakati, na mafanikio yake yatategemea usimamizi madhubuti.
"Hakikisheni huduma hii inaimarishwa na inaboreshwa mara kwa mara ili ikidhi mahitaji ya wateja katika mazingira yanayobadilika kila siku", alisema Waziri Silaa.
Waziri Silaa alisisitiza kuwa Shirika la Posta linapaswa kuweka mifumo thabiti ya kusimamia madereva wa bodaboda na watoa huduma wengine. Amelitaka shirika hilo kuhakikisha kuwa madereva wa bodaboda wanasajiliwa rasmi kwenye huduma hii, wanaelimishwa kuhusu maadili ya kazi, na kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
"Hakikisha kuwa mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo na vifurushi (real-time tracking) unafanya kazi kikamilifu na unatoa taarifa sahihi kwa wateja. Pia, epukeni ucheleweshaji wa huduma, kwani hii itajenga imani kwa wateja," alielekeza Waziri Silaa.
Pia, Waziri Silaa aliliagiza Shirika la Posta kuandaa programu za mafunzo kwa watoa huduma ili kuwajengea uwezo wa kutumia huduma ya Swifpack kwa ufanisi na kuwapa ujuzi zaidi kuhusu utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Waziri Silaa alisisitiza kuwa ili huduma hii iwe endelevu, Shirika la Posta linapaswa kuendelea kushirikiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali wa teknolojia ili kuhakikisha mfumo huu unafika maeneo mengi zaidi na kuhudumia wananchi wengi zaidi nchini.