Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI SILAA AMEIPA MIEZI MINNE BODI YA UCSAF KUSIMAMIA UKAMILISHAJI WA UJENZI WA MINARA 758


Na Mwandishi Wetu, WMTH Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) ameielekeza Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 unakamilika ndani ya miezi minne kuanzia sasa.

Waziri Silaa amesema unahitajika ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa mradi huo na uwe kipaumbele namba moja katika majukumu ya Bodi hiyo.

Ametoa maelekezo hayo leo tarehe 4 Februari, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo iliyofanyika ofisi za UCSAF, jijini Dodoma na kuongeza kuwa hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2025 minara iliyowashwa ni asilimia 50 (yaani minara 380 kati ya 758).

“Kwa kipindi hiki, Mfuko umepewa jukumu kubwa na la kimkakati ambalo lilishuhudiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo mnatekeleza mradi utakaowezesha taifa letu kupiga hatua zaidi katika kukuza uchumi wa kidijitali,” amesema Waziri Silaa.

“Kwa kuangalia muda uliobaki wa miezi minne (4), ni lazima mfanye jitihada kubwa kwa kuwasimamia watoa huduma ili kukamilisha mradi huu kwa wakati na kwa ufanisi,”amesisitiza Waziri Silaa.

Pia, ameitaka Bodi hiyo kuangalia namna bora ya Teknolojia itakayotumika kusimamia na kufuatilia minara inayojengwa na watoa huduma ili kuhakikisha inafanya kazi wakati wote.

Aidha, Waziri Silaa ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inashirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuona namna bora ya kukabiliana na changamoto za hali ya mawasiliano mipakani.

Vilevile, Waziri Silaa amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa ofisi za kanda ili ziweze kuwasaidia katika kupunguza malalamiko au changamoto zinazojitokeza kwa wakati.

"Ofisi hizi lazima ziwe na wataalamu wa kutosha na wafanye kazi kwa ukaribu na Halmashauri na viongozi wa mikoa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kupunguza kero kwa wananchi," amesema Waziri Silaa.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya wajumbe wa bodi, Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF, Mhe. Balozi Valentino Mlowola ameahidi kushirikiana na wadau wa sekta ya mawasiliano na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha UCSAF inaendelea kuwa chombo madhubuti cha kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya Mawasiliano.

“Tunaelewa kuwa jukumu letu ni kubwa na linahitaji umakini wa hali ya juu. Hata hivyo, kwa kushirikiana na timu ya menejimenti ya UCSAF, tutahakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinatumika kwa ufanisi mkubwa ili kufanikisha miradi inayolenga kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yale yasiyo na mvuto wa kibiashara,” amesema Mhe. Balozi Mlowola.