Habari
WAZIRI SILAA AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA OFISI ZA TCRA DODOMA

Na Faraja Mpina, WHMTH, Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha usimamizi wa ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo lililopo Njedengwa jijini Dodoma unafanyika hatua kwa hatua ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo leo Agosti 9, 2024 amesema inapotokea utekelezaji upo nje ya muda inamaanisha haijatokea ghafla bali kuna kazi ya siku moja iliingia kwenye siku nyingine na mwisho wa siku kutoka nje ya muda.
Wito wangu kila mtu atimize wajibu wake kwa kuzingatia takwa la kuhamia Dodoma ili ikiwezekana kuwe na mipango ya kukamilisha jengo la ofisi kabla ya muda uliopangwa bila kuathiri masuala ya kitaalamu ili Mamlaka iweze kuhamia Dodoma mapema zaidi.
Aidha, Waziri Silaa ameridhishwa na kazi nzuri inayofanyika na kuwataka kuendelea kusimamia ujenzi huo kwa uzalendo mkubwa kwasababu kukiwa na asilimia 10 tu ya utepetevu maana yake kuna asilimia 10 za kasoro zitakazoonekana katika jengo hilo.
“Msitu unatengenezwa na mti mmoja mmoja,hivyo kila mmoja wetu hapa ni mti mmoja mmoja kwenye msitu, kila mtu akitimiza wajibu basi tunakuwa na msitu imara wa pamoja”, amezungumza Waziri Silaa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, DKt. Jabir Bakari ameahidi kuhakikisha wanafanya kila kinachowezekana kwenda na kasi inayotakiwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwasilishaqa taarifa za maendeleo ya mradi mara kwa mara.