Habari
Waziri Kairuki ateta na wenyeviti wa bodi za taasisi zilizopo chini ya Wizara.
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Wenyeviti wa Bodi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara anayoiongoza kwa lengo la kujitambulisha na kuimarisha usimamizi na uwajibikaji wa taasisi hizo kwa manufaa ya taifa.
Mhe. Kairuki amewapongeza Wenyeviti hao kwa usimamizi mzuri kwa taasisi na kuwataka kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), pamoja na hotuba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Bungeni ili kila taasisi iweze kutambua wajibu na mchango wake katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo kupitia TEHAMA.
Na kusisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia bodi kufuatilia utendaji kwa mujibu wa sheria na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akitoa maelezo ya utangulizi katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, alitoa utambulisho wa Wajumbe wa Bodi na kueleza kwa ufupi uanzishwaji wa taasisi hizo kupitia sheria mbalimbali na kuonesha namna wizara inavyoshirikiana na taasisi hizo kupitia kamati za ushauri katika kusimamia maendeleo ya sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini.
Aidha, Mhe. Kairuki amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Bodi na Menejimenti ya Wizara. Na kuwakumbusha pia maelekezo aliyoyatoa kwa kila taasisi wakati wa ziara yake ya kikazi hivi karibuni ikiwemo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Taasisi, kuhakikisha mifumo ya TEHAMA inasomana, kutangaza huduma za taasisi kama vile Swift Pack ya Shirika la Posta, pamoja na kusimamia maboresho ya mbalimbali ya huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Amezitaka taasisi pia kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji yatakayoongeza mapato na kuimarisha ustahimilivu wao katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Akihitimisha, Mhe. Kairuki amewasisitiza Wenyeviti wa Bodi kuongoza mabadiliko ya kidijitali kwa kutumia teknolojia katika uendeshaji wa taasisi, sambamba na kuhamasisha watumishi kutumia TEHAMA katika shughuli zao za kila siku.
