Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATANZANIA KUWEZESHWA KUMILIKI SIMU JANJA


Na Chedaiwe Msuya

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema serikali iko mbioni kutafuta namna ya kumuwezesha mtanzania wa kawaida kumudu gharama ya kununua simu janja.

Hayo ameyasema wakati akizindua mnara wa kampuni ya Vodacom katika Kijiji cha Kinenulo kata ya Imalinyi mkoani Njombe.

Nnauye alisema kuwa hivi sasa wanafanya mazungumzo na makampuni ya simu."Na Mimi kwa sababu naipenda kazi yangu nimeshaanza kuangaika tumebanana na makampuni ya simu tunatafuta utaratibu ambao makampuni ya simu na watoa huduma wengine wataleta simu walau iwe ni kwa mkopo mtu alipe taratibu lakini aipate huduma aanze kutumia"alisema.

Aliongeza kuwa"Maana yake mtu wa kawaida kuchukua laki tatu ukaenda kununua simu kidogo ngumu lakini tukimwambia weka elfu 30,000 upewe simu ya laki tatu alafu utakua unakatwa kidogo kidogo hata kama ni kwa mwaka mzima,huduma unapata,umepata kwa bei ndogo na maisha yanaendelea maagizo hayo ameyatoa Rais Samia"alisema.

Alisema endapo kila mtanzania atakua na simu janja biashara itakua,kodi zitalipwa vizuri na huduma zitafanyika.

"Kwa hiyo ni matumaini yangu kuwapo kwa miundombinu ya mawasiliano kutaendana na kuwapo na vifaa vya mawasiliano alafu kutaendana na urahisi wa kuwasiliana"alisema Nnauye.

Hata hivyo Nnauye alisema kuwa malengo ya serikali ni kuhakikisha kila mtanzania kokote alipo anaunganishwa na huduma ya mawasiliano.

"Dunia ya leo mawasiliano ni kila kitu,ukizungumza elimu,ukizungumza afya,ukizugumza biashara,ukizungumza huduma za kifedha yote haya ukiwa na mnara hivi mambo yanakwenda sawasawa"alisema Nnauye.

Afisa mtendaji mkuu wa mfuko wa mawasilino kwa wote (UCSAF) Justina Mashiba,alisema wanajukumu la kupeleka huduma za mawasiliano vijijini na tayari wamejenga minara 1,087.

"Mkoa wa Njombe tunamiradi 32,minara 32 katika hiyo minara 30 imekamilika na miwili ipo katika hatua mbalimbali utekelezaji na ruzuku iliyotolewa na serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote ni bilioni 4.8 ndo imetumika kwa ajili ya kupeleka kama ruzuku kwenye miundombinu ya mawasilino"alisema Mashiba.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka alimueleza Waziri kwamba Halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto ya kukosekana ofisi ya sanduku la barua(posta).

Diwani wa kata ya Imalinyi Onesmo Lyandala aliishukuru serikali ya Rais Samia kwa kutatua changamoto ya mawasiliano ambayo ilikua ikiwakabili na kwamba maendeleo yatakwenda kwa kasi.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kinenulo Veronica John alisema uzinduzi wa mnara huo utawasaidia kurahisisha kughuli za mawasiliano ambapo hapo awali walikua wakienda umbali mrefu kutafuta mtandao.