Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATAALAMU UGANDA WAPONGEZA MAENDELEO SEKTA YA MAWASILIANO NCHINI


 

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, DODOMA

Timu ya wataalamu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekutana na kubadilishana ujuzi na timu ya wanasheria kutoka wa Wizara ya TEHAMA na Mwongozo wa Kitaifa pamoja na Tume ya Mawasiliano ya nchini Uganda waliokuja nchini kwa lengo la kujifunza ili kuboresha mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa Sekta ya TEHAMA nchini Uganda.

Akizungumza baada ya kikao kazi kilichofanyika Novemba 28, 2022 Wizarani jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo na Huduma za TEHAMA wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku amesema kuwa ugeni huo unaonesha kuwa nchi ya Tanzania imepiga hatua na inafanya vizuri katika sekta ya Mawasiliano na TEHAMA.

“Maeneo ambayo wataalamu hao wamekuja kujifunza ni maeneo ya uandaaji wa Sera, Sheria na Kanuni zinazoongoza sekta ya mawasiliano, utangazaji, huduma za posta na TEHAMA kwa ujumla”, amesema Munaku

Ameongeza kuwa, eneo jingine ambalo wataalamu hao wamekuja kuchukua ujuzi ni suala la mahusiano na ushirikiano baina ya Wizara na taasisi nyingine za Serikali zikiwemo taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na wadau wengine katika uandaaji na utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za Sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA.

Sambamba na kujifunza ujumbe huo pia umeonesha utayari na kuahidi kushirikiana na Tanzania kwenye matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kuandaa sheria na kanuni hasa kutokana na uthubutu wa Tanzania kuweza kutunga na kuandaa Sheria na Kanuni kwa lugha ya Kiswahili.

Wataalamu hao kutoka Uganda pia walifanikiwa kutembelea taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliyo chini ya Wizara yenye Makao Makuu yake jijini Dodoma.

Mkuu wa Idara ya Ununuzi na Ugavi wa UCSAF, Bw. John Munkondya akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF amesema kuwa dhumuni kubwa la ugeni huo ilikuwa ni kubadilishana uzoefu na kujifunza uendeshaji wa miradi ya mawasiliano, vifaa vya TEHAMA na utoaji wa mafunzo ya TEHAMA.

Akizungumza kwa niaba ya wataalamu kutoka Uganda, Bi. Susan Wegoye amesema kuwa ameshukuru kwa ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa Wizara pamoja na Taasisi yake ya UCSAF kwa kuweza kubadilishana uzoefu na kujifunza hasa kutokana na mabadiliko ambayo nchi ya Uganda inatarajia kuyafanya katika kuboresha sekta ya mawasiliano na TEHAMA nchini humo.

Ujumbe huo kutoka Uganda utakuwa nchini kwa ziara ya kikazi tarehe 28 Novemba hadi tarehe 2 Desemba ukiongozwa na Waziri TEHAMA na Mwongozo wa Kitaifa Mhe. Godfrey Baluku Kabbyanga na kupokelewa na Mhe. Nape Nnauye(Mb), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Novemba 28, 2022 jijini Dar es Salaam. Ujumbe huo pia utatembelea taasisi za TCRA, TBC, COSOTA na FTC kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.