Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANANCHI WASISITIZWA KUFANYA UHAKIKI WA LAINI ZA SIMU


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya uhakiki wa laini za simu kwa lengo la kutambua laini zilizosajiliwa kwa majina yao ili kuepuka kuhusishwa na makosa ya utapeli mitandaoni.

 

Hayo ameyazungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa tovuti na Mpango mkakati wa Wizara hiyo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26 uliofanyika jijini Dodoma

 

Amesema kuwa  ni muhimu kwa kila mwananchi kuepuka kusajili laini kwa kuweka alama ya kidole zaidi ya mara moja ili kuzuia usajili wa laini nyingine za ziada ambazo zinaweza kutumika kufanya uhalifu mitandaoni

 

“Wananchi wengi wamekuwa wahanga wa utapeli mitandaoni hivyo Wizara imejipanga kuimarisha mifumo ya kulinda faragha na taarifa binafsi ili zisitumike vibaya na watu wasiokuwa na nia njema”, alizungumza Dkt. Ndugulile

 

Aidha, amewaasa wananchi kuacha kutoa taarifa binafsi au kufuata maelekezo yeyote kwa watu wanaopiga simu na kujitambulisha wanatoka dawati la huduma kwa mteja katika makampuni ya simu ili kuepuka kutapeliwa

 

Ameongeza kuwa namba wanayotakiwa kupigiwa na makampuni ya simu ni namba 100 na sio kupigiwa na namba kutoka mitandao tofauti na mitandao wanayotumia huku wakijitambulisha wametoka huduma kwamteja na kuomba taarifa zao za kifedha au kutaka kujua salio lililopo katika laini zao za simu.