Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO KUPELEKWA MAFUNZONI


Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), amesema Serikali, kupitia Wizara anayoiongoza na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, itawezesha mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa waandishi wa habari za michezo kwa ajili ya fainali za AFCON 2027.

Akifungua TASWA Media Day Bonanza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), katika viwanja vya Msasani Beach Club, Dar es Salaam, Februari 10, 2024, Waziri Nape alisema, 'Serikali kupitia Wizara ya Habari na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tutandaa mafunzo pamoja na safari za nje ya nchi kwa waandishi wa habari za michezo ili kujiandaa vizuri katika kutoa habari za mashindano ya AFCON 2027.'

Aliongeza, 'Wanahabari ni watu muhimu katika kutangaza nchi yetu. Tunapenda kuwapa mafunzo na vifaa ili waweze kutangaza mashindano hayo kwa ufanisi.

Pia, nawasihi wanahabari wa michezo kufanya mazoezi ili kuhakikisha afya zao zinalindwa.'

Aidha, Waziri Nape aliwataka wanahabari kuepuka kuandika habari zinazowavunja moyo wanamichezo wa Tanzania, akisisitiza kuwa michezo ni mchanganyiko wa mafanikio na changamoto, hivyo ni muhimu kutoa msaada na uungwaji mkono kwa wanamichezo wetu.

"Tusiandike habari zinazowavunja moyo wanamichezo wetu," alisisitiza Waziri Nape, akitoa wito kwa waandishi wa habari za michezo.