Habari
Ujuzi na Maarifa Mtakayopata Usaidie kutekeleza malengo ya Serikali- KM Abdulla
Na Mwandishi Wetu, WHMTH Dodoma
Watumishi wa umma waliopata ufadhili wa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nje ya nchi wametakiwa kutumia vizuri fursa ya maarifa na ujuzi walioupata nje ya nchi kutekeleza malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku wakitambua kwamba chanzo pekee cha mafanikio ni ujuzi na uzoefu.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla tarehe 12 Julai, 2024 wakati wa hafla ya utoaji vyeti kwa wataalam 30 wa TEHAMA waliopata Ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali kwa mwaka 2024.
“Ufadhili huu ni wa kimkakati na tunatarajia kuwa, vijana waliochaguliwa watatumia fursa hii kujifunza, kushirikiana na wenzao walioko ng’ambo (nje ya nchi) na hivyo kuboresha weledi na maarifa katika utendaji kazi wao baada ya kuhitimu mafunzo yao ili kulifaidisha Taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Abdulla.
Katibu Mkuu Abdulla alisisitiza kwamba zoezi la ufadhili wa mafunzo kwa wataalam wa TEHAMA linatoa taswira ya dhamira nzima ya jukumu la wizara hiyo katika kukuza uwezo na ubunifu wa wataalam wa TEHAMA nchini.
Kupitia mradi huo jumla ya watumishi wa Serikali 500 watanufaika na programu hiyo kwa kushiriki mafunzo ya muda mfupi na mrefu.
Kwa upande wa mafunzo ya muda mfupi, ufadhili huo unaotolewa kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali hadi sasa umeshatoa wanufaika 50 ambao watapata shahada za uzamili katika maeneo mbalimbali katika nchi za Uingereza, Ujerumani, Marekani, Malaysia, Uturuki, Sweden na India.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naishukuru Benki ya Dunia kwa kuwezesha ufadhili huu nje ya nchi kwa watumishi wa Serikali," amesema Bw. Abdulla.