Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TEHAMA KUCHANGIA KATIKA SEKTA ZOTE ZA UCHUMI


Na Chedaiwe Msuya, WHMTH 

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema iko kwenye hatua za ukamilishwaji wa Mkakati wa uchumi wa Kidijitali (National Digital Economy Framework) ambao una lengo la kukuza matumizi ya TEHAMA kwenye sekta zote za uchumi ikiwemo kwenye uzalishaji wa bidhaa viwandani. 


Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Jim Yonazi katika hafla ya siku ya TEHAMA kwenye Maonyesho ya 7 ya Bidhaa za viwandani nchini ambapo amesema kuwa Matumizi ya TEHAMA yatasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza uzalishaji wa bidhaa za ndani,kuongeza ufanisi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kusambazwa kwa watumaji.

"Nitumie fursa hii kuwasisitiza matumizi ya TEHAMA kwenye uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa ujumla ili kuweza kuhudumia wateja wa hapa nchini pamoja na kutumia fursa za uwepo wa Soko hasa nchi jirani na kwenye Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Bara la Afrika (SADC) " Amesisitiza Dkt Jim Yonazi

Sambamba na hayo, Dkt Jim Yonazi amesema Mapinduzi ya nne ya Viwanda (4th Industrial Revolution) yanalenga matumizi makubwa ya kiteknolojia na data kama vile artificial intelligence, robotics, cloud computing, data centres, na mifumo mbali mbali ambayo kwa namna moja huongeza ustawi na ufanisi wa uendeshaji wa viwanda. 

"katika siku hii ya TEHAMA tungependa kuwakaribisha Wadau wote kuja kujifunza, kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu wa teknolojia mbalimbali zinazohusiana na ukuzaji wa maendeleo ya Viwanda na Biashara" Amesema Dkt Jim yonazi

Hata hivyo,katibu Mkuu huyo amesema Ajira za siku zijazo zitachochewa na teknolojia na uvumbuzi ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 65 ya watoto wanaoingia shule ya msingi leo watahitaji kazi ambazo bado hazipo (ITU,2022). 

"Takwimu hizi zinatilia mkazo kuwa miundombinu ya TEHAMA na mawasiliano ni nyezo kuu ya mapinduzi ya kidijitali kwenye sekta zote muhimu za uchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama na leo hii tunashuhudia mustakabali wa teknolojia na mitindo mipya ya mazingira ya biashara na kijamii kama vile biashara mtandao na hivyo tuweze kutafakari kwa kina namna ya kukuza, kuboresha na kufanya viwanda au biashara yako kuwa tayari kwa siku zijazo sasa" Amesema Dkt Jim yonaz.

Wadau  zaidi ya 500 wanaozungumzia ajenda mbalimbali za masuala ya Viwanda na Biashara wamekutana leo katika siku ya TEHAMA kwenye Maonyesho ya 7 ya Bidhaa za viwandani nchini yaliyofanyika  katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar esalam ambapo ajenda hizo kwa namna moja au nyingine haziepuki matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.