Habari
TANZANIA YAWEKA HISTORIA, YATWAA TUZO YA NYOTA INAYONG’AA KATIKA MAENDELEO YA POSTA DUNIANI.
📍 *BERNE, USWISI*
🗓️ Oktoba 2026
Tanzania imeweka historia katika sekta ya posta Duniani baada ya kutwaa tuzo ya Nyota Inayong’aa (*Rising Star*) ya mwaka 2026, inayotolewa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) kwa nchi zilizofanya maboresho makubwa katika maendeleo ya huduma za posta.
Tuzo hiyo imetolewa kupitia Kiashiria Jumuishi cha Maendeleo ya Posta (*Integrated Index for Postal Development – 2IPD*), kilichotathmini maendeleo ya sekta ya posta katika nchi 181 Duniani.
Aidha katika tukio hilo, Tuzo hiyo imepokelewa na Mhe. Angellah Kairuki (Mb), Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa niaba ya Tanzania, katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani iliyofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Duniani( UPU) Jijini Berne, Uswisi.
Utambuzi huu ni kutokana na juhudi za kuendeleza sekta ya posta kwa kuzingatia nguzo nne za Kielezo Jumuishi cha Maendeleo ya Posta (2IPD), ambazo ni uhakika wa huduma, umuhimu wa huduma na ustahimilivu.
Tuzo hii ina maana kuwa kichocheo cha kuongeza bidii katika maeneo yote manne yaliyopimwa. Pia inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa huduma za posta zinaendelea kuwa na umuhimu kama kichocheo cha ujumuishaji wa kidijitali, kifedha na kijamii, kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
