Habari
TANZANIA YASHIRIKISHA DRC UZOEFU WA KUIMARISHA SEKTA YA MAWASILIANO.
Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeshirikisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) uzoefu wake katika uandaaji wa sera, usimamizi wa Serikali, utekelezaji wa Sera ya Huduma kwa Wote na uratibu wa huduma za mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), katika kikao cha kubadilishana uzoefu kilichofanyika tarehe 6 Oktoba 2026, katika Ukumbi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano, Mhandisi Edith Turuka, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Mpango wa Anwani za Makazi (NaPA) na ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI) kinachojengwa Nala, Dodoma.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF), Bw. Mulembwa Denis Munaku, amesema maboresho yaliyofanywa katika sekta ya mawasiliano, hususan maeneo ya vijijini, yamechangia kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na matumizi ya huduma za kidijitali. Amesema Tanzania inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 wananchi wote wanakuwa wamefikiwa na huduma za mawasiliano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wote kutoka DRC, Bw. Christian Kavulu, amesema wamefika Tanzania kujifunza kutokana na uzoefu na mafanikio yaliyopatikana ili kuharakisha utekelezaji wa mipango ya mawasiliano nchini humo. Mkutano huo umebainisha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya mawasiliano na uchumi wa kidijitali.
