Habari
TANZANIA YAENDELEZA USHIRIKIANO NA ITU KWA MAENDELEO YA KIDIJITALI YA AFRIKA

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Geneva
Serikali ya Tanzania imebainisha dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kwa lengo la kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu ya kidijitali barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa alipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Mawasiliano Duniani zilizopo Geneva nchini Uswisi tarehe 06 Julai, 2025 na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) Bi. Doreen Bogdan – Martin.
“Tanzania pia inajivunia kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao la Afrika (Africa IGF) na Mapitio ya Kikanda ya WSIS+20, ikidhamiria kusimamia kwa pamoja sauti ya Afrika katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mustakabali wa kidijitali”, amesema Waziri Silaa.
Ameongeza kuwa, bado kuna pengo la muunganisho wa mtandao kwa asilimia 30 ya Watanzania walioko maeneo ya vijijini, hivyo inahitaji usaidizi zaidi katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano ya mwisho (last-mile connectivity).
Katika nyanja ya ubunifu wa ndani, Tanzania imefanikiwa kuanzisha mifumo muhimu kama Jamii Namba kwa utambulisho wa kidijitali, Jamii Malipo kwa huduma za kifedha, na Jamii Hub kwa kubadilishana taarifa kati ya sekta mbalimbali kwa usalama na ufanisi.
Vilevile, Serikali inaendelea kuanzisha vituo vipya nane vya ubunifu kote nchini, kuimarisha uwezo wa kitaifa kwenye teknolojia ya AI, pamoja na kukamilisha Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mtandao.
Aidha, hadi sasa, shule 1,300 zimeunganishwa na mtandao wa intaneti katika juhudi za kuharakisha mabadiliko ya kidijitali katika sekta ya elimu, huku Serikali ikihitaji msaada zaidi ili kuhakikisha shule zote nchini zinaunganishwa.
Waziri Silaa amesema, Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na ITU na washirika wengine wa maendeleo ili kujenga jamii ya kidijitali yenye usawa, ubunifu na ustahimilivu kwa Afrika na dunia nzima.