Habari
TANZANIA NA KONGO DRC KUSHIRIKIANA KATIKA TEHAMA
Na Chedaiwe Msuya, DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema inatarajia kuingia makubaliano na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuiunganisha katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuboresha huduma za mawasiliano nchini humo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Kongamano la Fursa za Kibiashara na Uwekezaji katika sekta ya mawasiliano linalotarajia kufanyika nchini humo kuanzia Oktoba 18-19, mwaka huu.
“Mbali na kongamano hilo, Serikali ya Tanzania itaingia makubaliano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kuunganishwa katika Mkongo wa Taifa utakaoboresha huduma za mawasilino ambapo kutaifanya nchi hiyo kuwa ya nane miongoni mwa nchi saba zilizounganishwa na Mkongo huo na kufungua fursa za kiuchumi na mapinduzi ya kidijiti,” amesema Nnauye.
“ Tanzania tumekuwa tukifanya vizuri katika utoaji wa huduma za mawasiliano tofauti na nchi nyingine, japo bado kuna baadhi ya changamoto lakini tumekuwa tukiendelea kuzitafutia ufumbuzi ,” alisema.
Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na waalikwa 300 na kampuni za 50 za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo wafanyabiashara wamehamasishwa kushiriki kongamano hilo kwa ajili ya kutangaza huduma za TEHAMA, kushiriki mijadala ya kukuza biashara, kujadili fursa za biashara, ubunifu na uwekezaji.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini, Bw. Kanupangi Gilbert alisema kuwa Tanzania na Kongo zimekuwa na uhusiano wa kindugu kwa muda mrefu na anaimani Kongamano hilo litaimarisha uhusiano uliopo.