Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA KUENDELEZA AJENDA YA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA - MHE. SILAA


Na Grace Semfuko, Maelezo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema, Serikali ya Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ajenda ya mabadiliko ya kidijitali na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, lengo likiwa ni kuwafikia watanzania wote katika sekta ya Mawasiliano.

Amesema sekta hiyo pamoja na kutoa ajira kwa vijana wengi, pia imekuwa ikisaidia kutatua matatizo katika jamii ikiwepo ya sekta ya afya ambapo kwa kuliona hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewekeza sana kwenye sekta ya Mawasiliano.

Mhe. Silaa ameeleza hayo leo 19 Septemba, 2024, katika fainali za shindano la Teknolojia la Marekani na Tanzania 2024 (U.S- Tanzania Tech Challenge 2024) lililofanyika Jijini Dar es Salaam.

"Serikali imekuwa ikielekeza na kuwezesha sekta ya mawasiliano, kupitia bajeti tuna uwekezaji mkubwa sana katika sekta hii, Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimeunganishwa vizuri na mawasiliano kupitia mkongo wa Taifa ambao upo Wilaya 109 kati ya 139, na sisi wizara ni wawezeshaji maana kupitia TEHAMA tunaweza kupata matibabu, masoko na mengineyo, kwa hiyo TEHAMA ni njia  kuwezesha sekta nyingine kukua, leo mkulima wa korosho Mtwara anaweza kutumia TEHAMA kupata mteja ndani na nje ya nchi", amesema Waziri Silaa.

Amesema pamoja na Tanzania kuwa na maendeleo makubwa katika kupanua huduma za mawasiliano, lakini pia inawezesha makundi maalum katika matumizi bora ya teknolojia ya kidijitali.

"Nchini Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na maendeleo makubwa katika kuendeleza ajenda ya mabadiliko ya kidigitali, maendeleo haya yamekuja pamoja na kupanua miundombinu na huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ikiwepo kuyaunganisha makundi ya wanawake na vijana katika matumizi bora ya kidigitali" amesema Mhe. Silaa.

Shindano hilo lililenga kuonesha ubunifu katika kutafuta suluhisho, na kuwafanya watu washiriki kwa kutumia Teknolojia katika kujenga uelewa, kuhusu dhima ya utendaji kazi wa vyombo vya habari nchini Tanzania ambapo mshindi wa kwanza ataibuka na zawadi ya Dola laki 2 za kimarekani.