Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU KIMATAIFA KWENYE USALAMA MTANDAO


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitisha tena ahadi zake pamoja na juhudi za pamoja katika kupambana na uhalifu wa kimtandao wa aina zote za uhalifu unaofanywa kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Uthibitisho huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bwana Selestine Gervas Kakele alipowasilisha tamko la Tanzania katika Kongamano la 17 la Kimataifa la Taasisi ya Kitaifa ya Usalama wa Taarifa Kimataifa (NAIIS) unaofanyika nchini Urusi.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua juhudi zilizochukuliwa na nchi mbalimbali na wadau wa kimataifa katika kuzuia matumizi mabaya ya TEHAMA kufanya uhalifu. Tanzania imejikita kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mifumo ya kitaasisi na kisheria ambayo lengo lake ni kuzuia na kupambana dhidi ya uhalifu wa kimtandao” amesema Bwana Kakele. 

“Miongoni mwa hatua tulizochukua ni kuandaa Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Mtandao, kupitisha sheria imara za usalama wa mtandao na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, Sekta binafsi, na Washirika wa kimataifa katika kubadilishana taarifa na uzoefu katika kukabiliana na changamoto zauhalifu wa mtandao” alisisitiza Bwana Kakele.

Aidha, amesema Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa usalama wa taarifa na TEHAMA kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. 

“Tunahimiza ushirikiano zaidi kati ya nchi na mashirika ya kimataifa ili kubuni na kutekeleza mikakati ya kukabiliana na vitisho vya kimtandao na kujenga uwezo wa kisheria na kiufundi”, alisema Kakele katika Tamko hilo.

Serikali ya Tanzania pia imeipongeza Urusi kwa kuandaa Kongamano hilo muhimu. “Tunajivunia kuwa sehemu ya jumuiya hii ya kimataifa inayohamasisha ushirikiano katika kukabiliana na uhalifu wa kimtandao” alimalizia Bwana Kakele, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano hilo.