Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI YAANZA KUWASHIRIKISHA WADAU KUHUSU MATUMIZI YA AKILI UNDE (AI)


Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo na Huduma za TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Angellina Misso, akizungumza na vyombo vya habari kuhusu matumizi ya akili unde (AI) nchini.

 

Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imefanya kikao na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi kwa ajili ya kujadili na kutathmini  utayari wa nchi katika matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI), kama hatua ya awali ya kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya AI.

Kikao hicho kilichoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kimefanyika Aprili 8, 2025 katika Hoteli ya Nashera, jijini Dodoma

Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo na Huduma za TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Angellina Misso amezungumzia lengo la kukutana na wadau ni kukusanya maoni yatakayoisaidia Serikali katika kuandaa mkakati bora na jumuishi wa matumizi ya teknolojia hiyo.

“Tuna watafiti wanaoangalia namna Akili Unde inaweza kusaidia katika sekta kama elimu, afya, kilimo, biashara na ulinzi. Kwa mfano, kupitia AI tunaweza kukusanya taarifa muhimu za wakulima, wagonjwa, wanafunzi na wafanyabiashara zitakazosaidia kutunga sera bora na kuelewa mahitaji halisi ya kila sekta,” alisema Dkt. Misso.

Kwa upande wake, Bi. Nancy Angulo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Ofisi ya UNESCO Tanzania, alisema shirika hilo linaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali kuhakikisha tathmini hiyo inakamilika kwa mafanikio.

“Kukamilika kwa tathmini hii kutaiwezesha Serikali kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuweka mikakati madhubuti ya matumizi salama na jumuishi ya teknolojia ya Akili Unde,” alisema Bi. Angulo.

Kikao hicho ni sehemu ya mchakato wa awali wa kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa AI ambao unatarajiwa kuhusisha mashauriano ya kina na wadau kutoka sekta mbalimbali, ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na mapinduzi ya teknolojia ya kidijitali kwa maendeleo endelevu ya taifa.