Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Serikali Yaahidi Kuboresha Sera na Miongozo ya Mawasiliano


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema Wizara hiyo itaendelea kuweka na kuboresha miongozo ya kisera na kisheria kwa lengo la kurahisha utoaji wa huduma kwa watumiaji wa mawasiliano nchini.

Amesema hayo tarehe 12 Julai, 2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya mashine saidizi (Personal Device Assistance – PDA) kwa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Bw. Abdulla amesema kuwa msaada huo ni ishara ya namna bora ya utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za taasisi za UCSAF na TPC katika kuhakikisha huduma za Mawasiliano ya Posta zinaboreshwa ili kuendana na mapinduzi yanayoendelea katika sekta hiyo.

“Kitendo cha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kulipatia Shirika la Posta Tanzania vitendea kazi hivi maarufu kama PDA, kutaimarisha uwezo wa Shirika kutoa huduma za usafirishaji kwa ufanisi na uhakika kote nchini,” amesema Abdulla.

Naye, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Maharage Chande ameushukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF kwa kuchangia maono ya TPC kwenda kidijitali kwani vifaa hivyo vitarahisisha sana utendaji kazi katika Shirika.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umelikabidhi Shirika la Posta Tanzania jumla ya mashine 250 zenye thamani ya shilingi milioni 216. Vifaa hivyo vitalisaidia Shirika la Posta Tanzania kutunza taarifa za wateja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

UCSAF na TPC ni taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zinazoendelea kuwezesha huduma ya mawasiliano ya simu na posta nchini.