Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUREKEBISHA KANUNI MBILI ZA SHERIA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeahidi kufanya marekebisho yote muhimu kama yalivyojadiliwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Kanuni mbili za Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) wakati akijibu hoja za Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge.

Naibu Waziri Mahundi amekiambia kikao hicho kilichoketi Ofisi za Bunge jijini Dodoma tarehe 09 Agosti, 2024, kwamba maboresho ya kanuni hizo yaliyowasilishwa leo na kujadiliwa yatazingatiwa kwa umuhimu mkubwa kwa maslahi ya taifa ili kupata taarifa iliyo sawa.  

“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wangu Mhe. Jerry William Silaa (Mb) tunaishukuru Kamati yako kwa kuendelea kuwa msaada katika kutimiza majukumu ya Wizara, na ninaahidi haya maboresho tuliyoyafanya hapa kwa umoja wetu, tunakwenda kuyazingatia na kuhakikisha taarifa iliyokamilika vizuri inawasilishwa,” amesema Naibu Waziri Mahundi.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Wizara Bi. Rehema Mpagama, amesema Kanuni zilizotakiwa kufanyiwa marekebisho ni mbili na kwamba zipo katika hatua ya ukusanyaji na uchakataji chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za kutangazwa.