Habari
SERIKALI KUONDOA VIKWAZO ILI BUNIFU ZITENGENEZE AJIRA KWA VIJANA

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Arusha.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) amesema Serikali ya Rais Samia haitoacha mawazo ya vijana wabunifu yapotee kwa kuwa kuna maeneo ambayo wakisaidiwa wataweza kuvuka vikwazo na mawazo hayo yanayoweza kutoa ajira kwa vijana.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi 13, 2025 wakati wa Mkutano wake na wadau wa kampuni changa (startups) na vijana wabunifu wa kidijitali uliofanyika katika jengo la Umoja wa Posta Afrika (PAPU Tower) jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya kupata maoni ya wadau ili kujua pengo la kisera lililopo la kusimamia, kulea na kuendeleza bunifu mbalimbali nchini.
Waziri Silaa amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kufungua milango kwa vijana wote wenye bunifu ili waweze kutambulika, kupata usimamizi na kukuza ndoto zao kwani wapo vijana wenye bunifu ambazo ni ngeni kwenye nchini na inakuwa ngumu kupata leseni kwa kazi wanazozifanya.
Amesema Wizara anayoiongoza pamoja na Tume ya TEHAMA ipo tayari kushirikiana na vijana wenye bunifu ili katika ngazi ya Serikali kuangalia namna bora ya kuweza kufanya kwa lengo la kuwaondolea vikwazo na kuwajengea mazingira wezeshi yakiwemo ya kisera ili kuweza kufikia malengo yao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema Serikali kupitia Tume hiyo inatoa fursa nyingi za ndani na nje ya nchi kwa vijana wabunifu kwa kuwaunganisha na wadau kupitia makongamano na majukwaa mengine ambayo vijana huonesha bunifu zao na kuvutia wawekezaji na mikopo ili kuweza kupata mitaji.
Kwa upande wa Dkt. Pamela Chogo, Mhadhiri kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) ameipongeza Wizara hiyo kwa kufanya mchakato wa utengenezaji wa sera ya kampuni changa kuwa shirikishi kwa kuwakusanya wadau ili kuchangia mawazo yao kushiriki katika hatua za awali za uandaaji wa sera hiyo.
Ameongeza kuwa juhudi hizo za Serikali zinaonesha kuwa changamoto nyingi zitatatuliwa na kuwasaidia vijana wenye bunifu kuweza kuzifanya kuwa biashara na kupata suluhisho za kiteknolojia na zisizo za kiteknolojia ambazo na kupitia sera na atamizi zilizopo za Serikali na binafsi watapata msaada ili bunifu zao zifike mbali zaidi.