Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUFIKISHA HUDUMA YA MAWASILIANO POTE NCHINI


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema Mkakati wa Serikali ni kufikisha huduma ya mawasiliano ya simu pote nchini kama ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 inavyoelekeza.

Mhandisi Kundo amesema hayo leo Bungeni Dodoma akijibu swali la Mhe. Samweli Hhayuma Mbunge wa Hanang kuhusu huduma za mawasiliano kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye.

Amesema kuwa, kampuni ya simu ya Tigo kwa ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Makangalimo kilichopo kata ya Sirop, Hanang.

“Kata ya Dirma yenye wakaazi takribani 8500 ambapo vijiji vitatu vya bassodesh, Qalosendo na Dirma yenyewe wanaenda kupata mawasiliano kupitia mtandao wa tigo na ndani ya mwezi huu mkandarasi ataanza ujenzi wa mradi huo”, amesisitiza Mhandisi Kundo

Aidha, amezitaja Kata za Gisambalag, Gehandu, Simbay na Gidahababieg kufanyiwa tathmini ya mahitaji halisi na kuingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa na UCSAF kulingana na upatikanaji wa fedha.

Sambamba na hilo, amezizungumzia kata ambazo hazina mawasiliano Mbulu Vijijini kuwa zimeingizwa kwenye mpango na utekelezaji wa miradi na watoa huduma wameshapatikana na tayari wanatekeleza mkataba wa miezi 24, akijimjibu Mhe. Flatei Massay (Mb.)wa Mbulu vijijini.