Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

SERIKALI KUCHUKUA HATUA KWA WALIOMZUSHIA KIFO MAKAMU WA RAIS


Na Mwandishi wetu, WHMTH, Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, ametangaza nia ya serikali kuchukua hatua za waliomzushia kifo Makamu wa Rais Dkt. Phillip Mpango, ili kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao na kuwalinda wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa X tarehe 10 Disemba 2023, Waziri Nape Nnauye alisisitiza kwamba serikali ina sheria zinazoelekeza matumizi sahihi ya mtandao pamoja na taasisi na watu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ili kulinda watumiaji mitandao na wananchi kwa ujumla.

 Aidha, Waziri amehakikishia umma kwamba hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia sheria hizo bila kuathiri uhuru wa watu, akionyesha matumaini kwamba wananchi wataelewa nia njema ya serikali katika kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao. Maoni yake yamepokelewa kwa namna tofauti na umma, huku baadhi wakitoa maoni yao kuhusu hatua hizo za udhibiti wa matumizi ya mtandao.

 Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa simu, Waziri Nape alisema kuwa matumizi salama ya mtandao ni muhimu sana katika kuhakikisha amani na usalama wa nchi unakuwepo. Amesema zipo sababu za msingi na umuhimu wa matumizi salama ya mtandao kwa kuepuka matumizi mabaya kama ilivyotokea hivi karibuni kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kumzushia kifo Mhe. Makamu wa Rais.

Akifafanua umuhimu wa kukuza amani na utulivu kwa nchi amesema “matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kusababisha taharuki na hata kuhatarisha amani na utulivu wa nchi. Kutoa taarifa za uzushi wa kifo kwa wananchi kunaweza kuchochea hofu na wasiwasi kwa jamii.”

Amesema pia kuwa kulinda heshima za wananchi wote, matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kudhuru sana heshima na hadhi ya wananchi kwa ujumla. Amefafanua kuwa kutoa taarifa na kuzusha kuhusu kifo kwa mtu yeyote ni ukiukwaji wa heshima na utu wa mtu na inaweza kuathiri maisha yao na kuleta mtafaruku usio na sababu.

“Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanaweza kutumiwa kwa urahisi kutengeneza na kusambaza habari potofu na za uongo. Kumzushia mtu kifo ni mojawapo ya mbinu zinazoweza kutumika kudanganya umma na kusababisha machafuko. Tunalazimika kama Serikali kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaovunja sheria za matumizi salama ya mtandao. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kujenga jamii inayoheshimu mawasiliano na inayofanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya maendeleo na amani ya nchi.” ameongeza Mhe. Waziri Nape Nnauye.

Mhe. Nape amesisitiza umuhimu wa kuwaheshimu na kulinda usalama wa viongozi na wananchi kwa kuhakikisha watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaheshimu maadili na kanuni pamoja na sheria za matumizi ya mawasiliano ikiwemo mitandao ya kijamii. “Matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa wananchi. Kutoa taarifa za uongo za kifo cha mtu,  kunaweza kusababisha taharuki kwa familia, ndugu na jamaa zake na wananchi kwa ujumla, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za kuzuia matendo kama haya” amesema Mhe. Nape.

Mhe. Nape pia amesisitiza umuhimu wa Serikali kuweka mazingira salama ya mawasiliano nchini ili kuhakikisha matumizi salama ya mtandao. “Tunaweza kujenga mazingira salama ya mawasiliano ambayo yanawawezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru bila kutumia njia za uongo na chuki kwa nia ya kudhalilisha na kuleta taharuki kwa jamii” amesema Mhe. Nape.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na taarifa kuhusu hali ya afya ya Mhe. Makamu wa Rais na kuleta mtafaruku mkubwa na hofu kwa wananchi na kwa familia yake. Serikali imekuwa ikiwakumbusha wananchi umuhimu matumizi salama ya mitandao kwa maendeleo badala ya kutumia vibaya. Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imekuwa ikitoa elimu kwa umma umuhimu wa matumizi salama, ikiwemo mwezi Oktoba 2023 ikiwa ni mwezi wa elimu kwa umma duniani kuhusu usalama wa matumizi ya mtandao.