Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU WAZIRI KUNDO AVITAKA VIJIJI KUILINDA MINARA YA MAWASILIANO


Na Immaculate Makilika – WHMTH

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa, Mhandisi Kundo Mathew amewataka wananchi wa Kata ya Mkula, Kijiji cha Katurukila kilichopo Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro kuilinda miundombinu ya mawasiliano katika maeneo yao kwa kuwa itasaidia kutoa ajira kwa mwananchi husika sambamba na kuchangia mapato katika Serikali za Vijiji.

Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekuwa ikitumia fedha nyingi kuijenga miundombinu hiyo ambapo gharama ya ujenzi wa mnara mmoja wa huduma za mawasiliano unakadiriwa kuwa takribani shilingi milioni 300 na kuwa gharama ya ujenzi huongezeka kutokana mazingira ya eneo husika.

Ameyasema hayo jana (Januari 7, 2023) wakati alipokuwa akihutubia wananchi wa Kijiji cha Katurukila kilichopo Kata ya Mkula mkoani Morogoro, wakati alipokuwa katika ziara yake kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano na kueleza nia ya Serikali ya kujenga minara saba ya huduma za mawasiliano jimboni hapo kwa lengo kutatua changamoto hiyo ya mawasiliano iliyopo.

“Minara itajengwa ndani ya jimbo na wilaya yenu hakikisheni mnakuwa walinzi wa minara yenu, walinzi wachaguliwe na Serikali za Vijiji na wasitoke katika mikoa au maeneo jirani, ulinzi wa minara ufanywe na Serikali za Vijiji ikiwa Mwenyekiti au Diwani hamtambui mlinzi aliyekuwepo basi achukuliwe hatua”, amesisitiza Mheshimiwa Naibu Waziri Kundo.

Mkazi wa Kijiji cha Mkuya, Kata ya Ipangalala, Bw. Godfrey Kipanda amesema kuwa uwepo wa minara ya mawasiliano katika maeneo yao sio tu inawapa faida ya mawasiliano bali inawasaidia wananchi kupata fedha kwa kuuza maeneo ambayo mnara utajengwa.

Naye, Mkazi wa Ifakara Mjini, Bw. Frank Mbise, amesema “ujenzi wa minara ya huduma za mawasiliano unasaidia kutupatia ajira kwa wananchi tunaoishi katika maeneo yenye minara hii. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kutuletea uwekezaji huu katika vijiji vyetu ili na sisi tupate mawasiliano na kukuza uchumi wetu kwa kufanya shughuli mbalimbali kupitia mawasiliano”.