Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

NAIBU KATIBU MKUU AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA UCSAF, ASISITIZA NIDHAMU NA UFANISI KAZINI


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa, ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya kazi na kuhamasisha watumishi kufanya kazi kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ili kuongeza ufanisi na kuimarisha ushirikiano kazini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Baraza la Pili la Wafanyakazi, iliyofanyika tarehe 18 Oktoba 2025 jijini Dar es Salaam, Bw. Mkapa alisisitiza kuwa mazingira bora ya kazi yana mchango mkubwa katika kuongeza tija na uwajibikaji wa watumishi. Aliongeza kuwa ni wajibu wa Baraza kusaidia kuweka mazingira yanayoruhusu maendeleo ya kitaaluma, ustawi wa watumishi na kuimarisha utamaduni wa utendaji bora katika taasisi.

“Baraza hili lisimame kama jukwaa la kujenga maelewano, lakini zaidi ya hapo, liwe kichocheo cha kuboresha mazingira ya kazi ili watumishi wawe na ari, ubunifu na ufanisi kazini,” alisema Bw. Mkapa.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, alisema kuwa Baraza hilo litakuwa chombo muhimu katika kufanikisha malengo ya Mfuko kwa kuwaunganisha wafanyakazi na kuwashirikisha kikamilifu katika mipango na maendeleo ya taasisi.

“UCSAF inaahidi kutumia maoni, ushauri na mawazo ya wafanyakazi wote kuboresha utendaji wake. Nitajitahidi kuhakikisha Baraza hili linakuwa huru na linafanya kazi zake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na masharti ya Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi tulioutia saini na Chama cha Wafanyakazi cha TUGHE,” alisema Mhandisi Mwasalyanda.

Uzinduzi wa Baraza hilo unafanyika kufuatia kukamilika kwa Baraza la Kwanza la Wafanyakazi la UCSAF, lililoanza mwaka 2022 na kuhitimishwa mwezi Juni 2025. Baraza jipya linatarajiwa kuendeleza misingi ya ushirikiano, uwazi na utawala bora katika mazingira ya kazi, sambamba na kuchochea ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya mawasiliano kwa wote nchini.