Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

MIAKA 61 YA UHURU NA INTANETI YA KASI KATIKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, KILIMANJARO

Katika kusheherekea miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia taasisi yake ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imefanikiwa kufikisha huduma ya mawasiliano ya intaneti ya kasi katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Wizara hiyo imeadhimisha siku ya Uhuru Disemba 9, 2022 kwa kupanda Mlima huo na kuzindua huduma hiyo iliyofikishwa umbali wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari na urefu wa kilomita 44.7 wa miundombinu ya mawasiliano iliyojengwa na TTCL kuanzia njia ya Marangu hadi Kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Uzinduzi huo umefanywa  na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Nape Moses Nnauye katika hafla fupi iliyofanyika katika geti la Marangu ukiwa ni mwanzo wa safari ya kuupanda Mlima huo na kwenda kuzindua huduma hiyo rasmi na mubashara akiwa katika kilele cha Mlima huo ifikapo Disemba 13, 2022.

Wizara hiyo mtambuka, wezeshi na ya kimkakati kupitia huduma zake za habari, mawasiliano na TEHAMA ina mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za kisekta na kukuza uchumi wa kidijiti.

Kwa kufikisha intaneti ya kasi katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro, Waziri Nape ameainisha faida kadhaa ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo ya hifadhi ya Mlima, idadi ya watalii itaongezeka na fursa za ajira pia zitaongezeka katika sekta ya utalii.

Aidha, Mawasiliano ya intaneti yenye kasi zaidi ya mbps 100 katika Mlima Kilimanjaro yatawawezesha watalii, wageni na watoa huduma katika Hifadhi ya Mlima huo kununua Vifurushi vya Intaneti kwa njia ya MasterCard, VISA, T-PESA na Mitandao mingine ya simu na malipo kufanyika kwa njia za kidijiti.

“Niwapongeze Shirika la TTCL kwa kufanikisha hili na kuweka historia, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatambua uzalendo na uwajibikaji uliofanywa na wataalamu wa TTCL, na hapa nitoe rai kwa vijana, tukio hili litumike kuamsha uzalendo na kujivunia kuwa wazawa wa nchi hii na kulitumikia Taifa hili kwa uzalendo mkubwa”, amezungumza Nnauye

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amelipongeza Shirika la TTCL kwa kutekeleza kwa vitendo dira ya Wizara hiyo ya kujenga Tanzania ya kidijiti kwa kufikisha huduma za intaneti ya kasi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga ameishukuru Wizara ya Maliasili na utalii na Wakuu wa Taasisi chini ya Wizara hiyo kwa ushirikiano na kuainisha maeneo ya hifadhi yenye uhitaji wa huduma za mawasiliano ambapo baada ya Mlima Kilimanjaro, TTCL itaanza kujenga miundombinu ya mawasiliano katika Hifadhi ya Mkomazi mwaka 2023.

Kamishna Mhifadhi wa Mlima Kilimanjaro, Dkt. Emilian Kihwele amesema kupanda mlima Kilimanjaro inachukua hadi siku sita hivyo jitihada zilizofanywa na Serikali za kutatua changamoto za mawasiliano katika mlima huo zitaongeza idadi ya wageni k na kuongeza pato la Taifa.