Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KAMPUNI ZA SIMU ZACHANGIA MILIONI 240 KUSAIDIA WAHANGA WA MAFURIKO HANANG’


Na Georgina Misama – WHMTH

Umoja wa Kampuni za Simu Tanzania (TAMNOA) zinazojumuisha Kampuni za TTCL, VODACOM, TIGO, AIRTEL na HALOTEL zimeitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuunga mkono juhudi za kusaidia wahanga wa mafuriko katika mkoa wa Manyara wilayani Hanang, Katesh kwa kuchangia shilingi milioni 240 kwa ajili ya kuwasaidia wahanga hao.

Akipokea misaada hiyo kwa niaba ya Serikali leo Desemba 4, 2023 jijini Dar es salaam, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewashukuru wawakilishi wa kampuni hizo za simu kwa wepesi wao wa kuitikia wito uliotolewa na Rais Dkt. Samia jana Desemba 3, 2023 na kwamba kampuni hizo zimeonyesha uzalendo mkubwa.

Mhe. Nape alisema kwa upande wa Serikali katika kuitikia wito wa Rais Samia, Wizara yake imetuma timu mkoani Manyara ili kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya mawasiliano na kwamba taarifa alizopokea hakuna uharibifu mkubwa, ambapo tayari hatua zimechukuliwa katika kurekebisha dosari ndogo zilizojitokeza ili kuhakikisha mawasiliano yanarejea katika hali yake mapema.

“Nipo hapa kuwashukuru umoja wa makampuni ya simu Tanzania kwa kuitikia wito wa Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa uzalendo wao wa kuamua kuwasidia wenzetu ambao wapo kwenye matatizo, kwa niaba ya Serikali nimekuja kuupokea mchango wao wa zaidi ya shilingi milioni 200, nawashukuru sana kwa kuitika kwa haraka na nawaahidi kwa niaba ya Serikali tutazifikisha Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia maafa ili ziwafikie walengwa,” alisema Mhe. Nape.

Alisema  fedha hizo zitaongeza kusaidia kuwarudishia wahanga wa mafuriko hayo maisha na kwamba anatoa wito kwa taasisi nyingine nchini kuendelea kusaidia kwani majanga kama haya hayapangwi hivyo yanapotokea ni vizuri kuungana pamoja na kusaidiana.

“Tumeunganisha nguvu zetu katika kipindi hiki kigumu ili kuunga mkono juhudi za Serikali na kwa umoja wetu tumeweza kuwasilisha shilingi milioni 240 kiasi hicho cha fedha kitasaidia kuwapatia wahanga mahitaji muhimu kama vile maji safi, chakula, mashuka na  wakati huu wa matatizo,” alisema Mwenyekiti  TAMNOA, Philip Besiimire.

Katika mafuriko hayo imeripotiwa watu 50 wamepoteza maisha  hadi kufikia Desemba 4, 2023 na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa ambapo kufuatia janga hilo Rais Samia akiwa safari ya kikazi Dubai alituma salamu za pole na kuelekeza mamlaka za Serikali  kuelekeza nguvu katika kuhakikisha misaada yote muhimu inapatikana.