Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

“JENGO LA PAPU LIKAMILIKE KWA MUJIBU WA MAKUBALIANO NA KWA UBORA WA KIMATAIFA” KATIBU MKUU WHMTH


Na Innocent Mungy, WHMTH, ARUSHA

Serikali imeagiza mradi wa jengo la Makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika (Pan African Post Uniuon PAPU) ukamilike kwa mujibu wa muda uliokubaliwa wa ujenzi wa mradi huo na kwa ubora wa kimataifa.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi wakati alipotembelea jengo hilo mapema wiki hii kukagua maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa ushirikiano kati PAPU pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Dkt. Yonazi alikuwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Umoja huo Bwana Sifundo Chief Moyo pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa mradi huo Bwana Victor Nkya. Dkt. Yonazi ametoa pongezi za Serikali kwa Menejimenti ya PAPU na TCRA kwa kusimamia kwa karibu ujenzi wa mradi huo mkubwa unaojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Posta Afrika (PAPU).

“Nimeona kazi nzuri inayofanyika, muda uliobaki sio mrefu, na Serikali haiwezi kusubiri muda mrefu Zaidi, naagiza maandalizi ya kuzindua jengo yaanze sasa kwa kuwa na kamati ya Uzinduzi wa jengo ili twende sawa na makubaliano na tukabidhi jengo kama tulivyokubaliana na katika ubora wa kimataifa” alisema Dr. Yonazi.

Aidha Dkt. Yonazi ameelekeza Kamati ya Ujenzi inayoratibiwa na TCRA pamoja na PAPU kuhakikisha kuwa wote waliohusika katika ujenzi wa mradi huu wa kihistoria ulioahidiwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya mwalimu Julius Nyerere kwa Bara la Afrika, majina yao yanawekwa kwa ajili ya kumbukumbu, yakiwemo ya Wakandarasi, watoa huduma mbalimbali na watu binafsi walioshiriki kujenga jengo hilo. Alisema kiandaliwe kitabu maalumu chenye majina ya wote walioshiriki kufanikisha mradi huo.

Nae Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika Bwana Sifundo Chief Moyo alimshukuru Dkt. Yonazi kwa kutembelea na kuona utekelezaji wa ujenzi wa jengo la PAPU (PAPU House) pamoja na mazingira ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa yanavyoendelea.

“Ujio wako leo ni wakati muafaka wakati tuanaelekea kukamilisha ujenzi wa jingo hili muhimu sana kwa Umoja wa Posta Afrika. Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ujenzi wa jingo hili kupitia Kamati ya Ujenzi inayosimamiwa na TCRA. Nimeona mabadiliko makubwa siku za hivi karibuni jinsi mradi huu unavyokaribia ukingoni; alisema Bwana Moyo.

Amemhakikishia Dkt. Yonazi kuwa kupitia eneo itakayowekwa makataba ya umoja huo, wote walioshiriki ujenzi wa jingo hilo watakumbukwa na kuwekwa kwenye kumbukumbu za PAPU katika Maktaba hiyo kupitia machapisho mbalimbali.

Jengo hilo linatarajiwa kukabidhiwa kwa matumizi kabla ya mwisho wa mwezi Machi 2023 baada ya ujenzi kuanza tarehe 18 Januari mwaka 2020. Ujenzi wa jengo hili ni ahadi iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya kwanza kwenye 1980 chini ya Mwalimu Julius Nyerere. Tanzania ni mwenyeji wa PAPU toka mwaka 1980 na jengo litakapokamilika PAPU itahamia katika jingo hilo litakalokuwa Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika, jijini Arusha.