Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

HUDUMA ZA MAWASILIANO KUWALETEA MAENDELEO WAKAZI WA IBIRI – MHANDISI MAHUNDI


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Tabora

Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema kuwa kuwepo kwa mnara wa Halotel katika Kata ya Ibiri kutachangia kukuza uchumi wa wakazi wa eneo hilo.

Naibu Waziri Mahundi aliyasema hayo tarehe 26 Machi 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya mawasiliano katika Kata ya Ibiri, Jimbo la Tabora Kusini.

“Kwakweli tunapata faraja tunapokuta huduma tunayoitoa inawaridhisha wananchi,” alisema Naibu Waziri Mahundi.

“Sote tunafahamu kuwa dunia ya sasa ni kijiji, hivyo ni lazima tuboreshe mawasiliano yetu. Pia, vijana wetu wanatumia mtandao kwa ajili ya kusoma, na ninyi wakulima wa tumbaku na alizeti mnaweza kutumia mtandao kujua soko la mazao yenu,” aliongeza.

Aidha, alieleza kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ilitoa zaidi ya shilingi milioni 145 kusaidia ujenzi wa mnara huo wa Halotel, ambao umegharimu jumla ya shilingi milioni 290.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Halotel Kanda ya Kati, Bw. Emmanuel Mahundi, alisema kuwa kampuni yao imeongeza kiasi cha shilingi milioni 145 kugharamia mradi huo. Mnara huo utahudumia Kata ya Ibiri pamoja na vijiji 8 vyenye wakazi wapatao 3,000 na una teknolojia za 2G, 3G na 4G.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mwakishinde, Bi. Salma Saidi, aliishukuru Serikali kwa hatua hiyo, akisema kuwa awali hakukuwa na mawasiliano katika eneo hilo. Alisema mnara huo utaboresha huduma mbalimbali kama usalama, mawasiliano ya dharura na biashara.

Mnara huo ni sehemu ya minara 758 inayojengwa kwa ruzuku ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) chini ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP).