Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. NDUGULILE ATEMBELEA MAONESHO YA MAKISATU DODOMA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ametembelea mabanda ya wabunifu mbalimbali kwenye Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

 

Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda ya wabunifu hao Dkt. Ndugulile ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kubuni mashindano ya MAKISATU ambayo yanasaidia kuvumbua vipaji na ubunifu uliopo ndani ya nchi

 

“Nimeona ubunifu mwingi katika maonesho haya na nimefurahishwa na ubunifu wa vijana wadogo, wengine wapo shule za msingi ambao wamekuja na majibu ya changamoto ambazo tunazo kwenye jamii”, alisema Dkt. Ndugulile

 

Aliongeza kuwa Wizara yake inafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya  Elimu, Sayansi na Teknolojia  na lengo la kwenda katika maonesho hayo ni  kuangalia ubunifu uliopo ili  kujipanga katika maonesho ya mwakani Wizara yake wasishiriki kama waalikwa bali Wizara hizo mbili zishirikiane kufanya maandalizi pamoja na ushiriki yakinifu.

 

Dkt. Ndugulile amezungumzia masuala ya ubunifu kama kipengele ambacho Wizara anayoisimamia inahusika moja kwa moja hasa kipengele cha ubunifu katika TEHAMA, na kuahidi kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  ili katika maeneo ambayo Wizara yake ina ushiriki waweze kuyatafutia ufumbuzi.

 

Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa ni muda muafaka wa kuangalia suala la ubunifu katika mtazamo mpya kama nchi kwa kuwajengea uwezo vijana wabunifu  waweze kutengeneza bidhaa na kuwatafutia masoko ili wauze bidhaa au kampuni walizozitengeneza na kwenda kufanya ubunifu mwingine mpya ili kuendelea kupiga hatua kama Taifa.