Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

ANWANI ZA MAKAZI KUSAIDIA KUPANUA WIGO WA BIASHARA


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Matumizi ya Anuani za Makazi kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali Wadogo nchini yametajwa kuwa ni moja ya njia za kuongeza wateja katika biashara mbalimbali zinazofanywa na wananchi.

Hayo yamezungumzwa leo jijini Dodoma na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo, Aloyce Mwangofi wakati akifungua mafunzo ya Anuani za Makazi yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa jumla ya Wafanyabiashara 100 wa mkoani hapo.

Mwangofi amesema kuwa wafanyabiashara ni watu muhimu kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi, pia ndio wanaokimbiza uchumi, hivyo wanatakiwa kupewa mafunzo mbalimbali yatakayowasaidia kukuza biashara zao.

"Anuani za Makazi ni hitaji la Kidunia, ni ongezeko la orodha ya vitu vinavyotambulisha, kwa Wafanyabiashara ni hatua ya kuongeza wateja bila kutumia nguvu nyingi. Lengo la mfanyabiashara sio tu kuuza biashara alizonazo lakini pia ni namna gani wateja wanaweza kumfikia", alisema Mwangofi.

Ameongeza kuwa, Dunia ya sasa ni ya kibiashara na biashara hizo zinafanyika zaidi kwa kuwasiliana, hivyo kwa kutumia Anuani za Makazi maelekezo yatakuwa ni ya kisayansi na kitaalamu na yatarahisisha utoaji huduma.

Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara hao kuuelewa vizuri mfumo huo kupitia mafunzo wanayopewa ili waweze kuwa mabalozi wazuri na kuweza kuwaelekeza wafanyabiashara wenzao matumizi ya mfumo huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa mbali na mafunzo ya Anuani za Makazi, katika kikao hicho wafanyabiashara wataelezwa pia kuhusu mifumo mingine ya kidijitali itakayowasaidia katika kuongeza wateja ikiwemo ya mitandao ya kijamii.

“Kama Wafanyabiashara tutatangaza biashara zetu huku tukitaja anuani kamili, tutaweza kupatikana kwa urahisi na hivyo kurahisisha biashara”, alisema Mhandisi Clarence.

Mfumo wa Anuani za Makazi ni miundombinu ambayo kwa pamoja inatambulisha mahali halisi mtu au kitu kilipo juu ya uso wa nchi, aina hii ya utambulisho inaundwa na vitu vitatu ambavyo ni; namba ya nyumba, jina la barabara na postikodi.