Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANAOKWAMISHA OPERESHENI YA ANWANI ZA MAKAZI KUCHUKULIWA HATUA


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua mwenendo wa utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi kwenye barabara, mitaa na nyumba mbalimbali katika Mkoa wa Tanga. Katikati mwenye kofia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Adam Malima.

TANGA.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kuhakikisha anawachukulia hatua wale watakaobainika kukwamisha utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi katika Mkoa huo

Akizungumza leo Jumatatu tarehe 11 Aprili, 2022 jijini Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua mwenendo wa utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Waziri Nape ameonesha kutokuridhishwa na kasi ya utekelezaji katika Mkoa huo unaoshika nafasi ya pili kutoka mwisho

“Hili la Operesheni ya Anwani za Makazi ni jambo letu sote, tuone shida ya kuwa mkiani, wanaotukwamisha washughulikiwe na kama kuna shida kwenye utekelezaji tuelezane tutatue kwa pamoja”, Amezungumza Waziri huyo

Waziri Nape amesisitiza kuwa uwekaji wa Anwani za Makazi sio zoezi la kawaida ni operesheni maalum iliyotangazwa na Rais, ambapo kukamilika kwake kutarahisisha kufanyika kwa sensa ya watu na makazi na ufikishaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Adam Malima amekiri utekelezaji wa Operesheni hiyo bado haujaanza katika halmashauri tatu za Mkoa huo, ambazo ni halmashauri ya Korogwe mji, Korogwe vijijini na Kilindi kutokana na changamoto za kiutendaji

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Mfumo wa kielektoniki unaoingiza taarifa za wakazi na makazi unafanya kazi vizuri, na Wizara hiyo ipo tayari kutoa wataalamu kwenda kuongeza nguvu kwenye mkoa au halmashauri yeyote ambayo ina uhitaji.