Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TANZANIA YATANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI WA TEKNOLOJIA KOREA KUSINI


Na Mwandishi Wetu – WMTH

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), 
amesema Tanzania imeanza mchakato wa kuandaa Mfumo wa Akili Unde wa Lugha kwa Kiswahili (LLM) ili kupanua matumizi ya Teknolojia hiyo katika elimu, afya, kilimo na huduma za umma.

Dkt. Mkama ameyasema tarehe 19 Oktoba, 2026 wakati akichangia mada kuhusu Akili Unde na Huduma za Kidijitali kwa Umma, katika Mkutano wa Kimataifa wa Akili Unde na Teknolojia za Kidijitali (Global AI & Digital Summit 2026), unaofanyika Seoul, Jamhuri ya Korea, kuanzia tarehe 19 hadi 22 Oktoba 2026.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine, taasisi za kimataifa na kampuni za teknolojia ili kuvutia uwekezaji, kupata utaalamu na kuendeleza teknolojia nchini.

Mkutano wa Kimataifa wa Akili Unde na Teknolojia za Kidijitali umeandaliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Korea, unalenga kujadili matumizi ya Akili Unde na teknolojia za kidijitali katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha huduma za umma.

Tanzania inatumia fursa ya mkutano huo kutangaza mradi wa Nala Techno Valley unaopangwa kujengwa Nala, Dodoma, katika eneo la ekari 400 zilizotengwa na Serikali. Mradi huo unalenga kuanzisha kitovu cha teknolojia, ubunifu, Akili Unde, roboti na kampuni changa za teknolojia.

Katika mkutano huo, Tanzania pia inaendelea kujenga ushirikiano na wadau wa kimataifa yatakayosaidia kupata washirika wa kimkakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya teknolojia. Juhudi hizo ni sehemu ya kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza mchango wa Teknolojia katika Maendeleo ya Taifa.