Habari
TANZANIA YAIMARISHA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA MITANDAO
Na Mwandishi Wetu
Tanzania inaendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kidijitali ni wa uhakika, endelevu na unaoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za mitandao.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb) wakati akichangia katika
Mjadala wa Ngazi ya Juu kuhusu Ustahimilivu uliowakutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mawasiliano duniani katika Mkutano wa ITU - PP 26 unaoendelea Doha, nchini Qatar.
Alisema kuwa, kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ya Kasi (NICTBB), Tanzania imejenga mfumo wa mawasiliano unaounganisha maeneo mbalimbali kwa njia mbadala (Mesh Network), unaofikia mikoa yote, wilaya 122 kati ya 139 na nchi saba jirani, hatua inayoongeza uimara na upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Waziri Kairuki aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania inaendelea kuwekeza katika vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa za kidijitali (Data Centres), kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, kutumia teknolojia za ufuatiliaji wa mitandao kwa wakati halisi na kuimarisha usalama wa miundombinu muhimu ya TEHAMA dhidi ya vitisho na mashambulizi ya kimtandao.
Hatua hizi zinalenga kuhakikisha huduma muhimu za Serikali, afya, elimu na fedha zinaendelea kupatikana hata wakati wa changamoto zinazoweza kuathiri mitandao ya mawasiliano.
Tanzania inaendelea kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu imara na salama ya kidijitali kama msingi wa uchumi wa kidijitali, maendeleo jumuishi na ustawi wa wananchi.
