Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TAMKO LA USHIRIKI WA TANZANIA KWENYE MWEZI WA ELIMU KWA UMMA YA USALAMA MTANDAO MWAKA 2023


Na Juma Wange

Mabadiliko ya kasi na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameleta mageuzi makubwa kwenye maeneo mengi ya Maisha yetu ikiwemo namna ya kuwasiliana, upatikanaji wa huduma mbalimbali kupitia mitandao, upatikanaji wa Habari, uwezo wa kufikia wateja wengi kwa muda mfupi na kuongezeka kwa tija katika maeneo mbalimbali ya kisekta na kiutendaji.

Pamoja na mafanikio mengi yaliyoletwa na TEHAMA, kumekuwepo na changamoto zinazosababishwa na watu wachache ambao wanatumia mitandao kutekeleza matukio ya kihalifu mtandaoni na hivyo kulazimu Serikali kuchukua jitihada za makusudi za kuhakikisha zinawalinda wananchi na anga ya mtandao ya nchi inakuwa salama.

Aidha, kwa kuwa anga ya mtandao haitambui mipaka ya kijiografia, changamoto ya uhalifu wa mtandao imekuwa ni agenda ya Kikanda na Kimataifa ambapo zimeanzishwa jitihada za mashirikiano katika usalama mtandao hususan katika miongozo ya utungwaji wa sheria za usalama mtandaoni, kujenga uwezo wa wataalam na kubadilishana uzoefu na mbinu za kukabiliana na uhalifu mtandaoni.

Nchini tumefanya mengi ikiwemo utungwaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015; na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022, zote hizo ni jitihada za Serikali kuweka mazingira mazuri ya anga ya mtandao nchini.

Pamoja na jitihada za kuhakikisha sheria zinakuwepo bado kuna mwanya mkubwa wa uhalifu mtandaoni unaosababishwa na udhaifu wa kibinadamu. Mathalani kuamini watu kwa haraka, kujisahau, kuwa wepesi kutaka kusaidia n.k.

Hivyo ili kuwalinda watumiaji wa mtandao ni muhimu kuwajengea uwelewa wa namna ya kuwa na matumizi salama ya huduma na bidhaa za TEHAMA. Katika jitihada za kuwalinda watumiaji wa mtandao, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Benki Kuu ya Tanzania na Wadau wengine kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi nchini inaungana na ulimwengu kuadhimisha Mwezi wa Elimu kwa Umma ya Usalama Mtandaoni ambao hufanyika mwezi Oktoba kila mwaka tangu mwaka 2004. Kwa maadhimisho ya mwaka huu 2023 Kauli mbiu ni “Ni rahisi kuwa Salama Mtandaoni”.

Lengo la kutoa elimu kwa umma ya matumizi salama ya mtandao kwa watu binafsi na taasisi ni kupunguza matukio ya uhalifu mtandaoni kwa kujenga uwelewa kuhusu mbinu zinazotumika kufanya uhalifu mtandaoni, namna wanavyoweza kubaini mashambulizi ya mtandao na masuala gani wanayoweza kufanya ili kujikinga dhidi ya uhalifu wa mtandao.
    
Tusaidiane kuelimishana na kukumbushana kuzingatia matumizi salama ya mtandao ili sote tuwe salama mtandaoni kwani kila mmoja akipata elimu hii nawahakikishia kuwa ni rahisi kuwa salama mtandaoni.
Aidha, katika maadhimisho ya mwaka huu, timu ya wataalam itazunguka katika baadhi ya mikoa yenye wahanga wengi wa uhalifu wa mtandao na kwa kushirikiana na Vyombo vya Habari nchini ili kuitoa elimu ya matumizi salama ya mtandao ili kuwezesha umma wa Watanzania kuwa salama mtandaoni. Baadhi ya masuala muhimu ambapo maadhimisho ya mwaka huu yatajikita ni pamoja na: -
• Kuwezesha “Multifactor Authentication” ili kulinda akaunti zetu mtandaoni;
• Matumizi ya nywira thabiti pamoja na programu za usimamizi wa nywira;
• Kusasisha programu zote za vifaa vya TEHAMA ikiwemo simu za viganjani, kompyuta n.k.;
• Futa “delete” kabisa;
• Kutambua na kuripoti kuhusu udanganyifu mtandaoni (Phishing);
• Ukipokea jumbe ya kitapeli au simu ya kitapeli itume kwenda namba 15040; na
• Usiamini simu ya mtoa huduma wa mawasiliano ambayo sio 100.
NAWATAKIA KILA LAKHERI KATIKA MATUMIZI BORA NA SALAMA YA MTANDAO.

“Ni Rahisi Kuwa Salama Mtandaoni"