Habari
SERIKALI YAIMARISHA UWEZO WA KITUO CHA TAIFA CHA KUHIFADHI DATA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni 39 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya mradi wa ununuzi wa vifaa pamoja na upanuzi wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data,
Waziri Kairuki ameyasema Hayo wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hatua zilizofikiwa katika ununuzi wa vifaa na upanuzi wa Kituo cha NIDC mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika Kikao kilichofanyika Bungeni, jijini Dodoma.
Amefafanua kuwa, Shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa utekelezaji wa Awamu ya Kwanza, itakayohusisha upanuzi wa eneo la kufunga mifumo ya TEHAMA, kuongeza vifaa maalumu vya kufungia mifumo (equipment racks) 42 pamoja na kubadilisha vifaa vilivyofikia ukomo wa muda wa matumizi.
Waziri Kairuki pia amewasilisha taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha kampuni za mawasiliano ya simu nchini zinajiorodhesha katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kwa mujibu wa matakwa yaliyowekwa, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wa wananchi katika umiliki wa kampuni hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb.), amesisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia maboresho yanayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya Wizara, hususan mradi wa kuongeza uwezo wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data za Mtandao, akieleza kuwa ni mradi muhimu wenye uhitaji mkubwa kwa Taifa.
Aidha, ameiipongeza Serikali kwa juhudi za kuimarisha huduma za mawasiliano kupitia ujenzi wa minara ya mawasiliano, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na mpango kazi endelevu wa kutafuta na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa minara zaidi, ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano kwa kuimarisha miundombinu ya kidijitali katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi zake ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
