Habari
RAIS SAMIA ASISITIZA MATUMIZI YA TEHAMA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI
Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kutatua changamoto za wananchi na kuboresha utoaji wa huduma za umma nchini.
Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 30, 2026, wakati akizindua rasmi matumizi ya majengo ya Wizara, Taasisi za Serikali na Barabara za lami katika Mji wa Serikali uliopo Mtumba, jijini Dodoma, baada ya kuvutiwa na mifumo ya TEHAMA iliyowekwa katika eneo hilo.
Amesema mifumo ya TEHAMA ya Serikali inapaswa kuunganishwa na kuwezesha mifumo hiyo kusomana ili kurahisisha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa, hatua itakayopunguza usumbufu kwa wananchi wa kuhitajika kuwasilisha taarifa zilezile katika taasisi mbalimbali za Serikali.
Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa upanuzi wa upatikanaji wa huduma za TEHAMA katika maeneo mengi nchini utarahisisha utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma yanapaswa kwenda sambamba na misingi ya haki, usawa na uadilifu ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora bila ubaguzi.
Vilevile, amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali wa Mtumba kutunza miundombinu na vifaa vilivyowekwa, ili viendelee kutoa huduma kwa ufanisi na kudumu kwa manufaa ya Serikali na wananchi kwa ujumla.
