Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT CHAULA AONGOZA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KUANDAA MPANGO MKAKATI WA UTENDAJI KAZI NA UFUATILIAJI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula ameongoza Menejimenti, maafisa waandamizi na wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kuandaa Mpango Mkakati wa utendaji kazi na ufuatiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, kazi itakayofanyika kwa siku 12 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.

 

Dkt Chaula amesema kuwa maandalizi ya kuandaa Mpango huo yalikuwa yamekwishafanyika  lakini msukumo mkubwa umetokana na kuundwa kwa Wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yanayoenda sambamba na mabadiliko ya kimuundo kulingana na mahitaji ya Wizara pamoja na kuongeza uwajibikaji wenye matokeo chanya.

 

“Mpango Mkakati huu tunaouandaa utarahisisha kupima utendaji wetu kama Wizara katika kufikia malengo, kujua  mchango halisi wa Wizara katika kuinua pato la Taifa na kujua maeneo ambayo Wizara imechangia pato hilo “, alizungumza Dkt Chaula

 

Ameongeza kuwa kazi ya kuandaa mpango huo inahitaji ushirikishaji, umakini na utulivu mkubwa ili kupata Mpango Mkakati bora, wenye viwango na wenye muda wa utekelezaji unaopimika na kusisitiza Mpango huo uwe  katika lugha ya Kiingereza  na Kiswahili.

 

Naye mwezeshaji wa kuandaa Mkakati huo Beltila Mgaya kutoka Ofisi Ya Rais Utumishi na Utawala Bora, amempongeza na kumshukuru Dkt Chaula kwa kushiriki na kuipa kipaumbele kazi hiyo ambayo baadhi ya Watendaji Wakuu wa Sekta ya umma huwa hawashiriki kwa karibu.

 

Ameongeza kuwa kazi hiyo itafanyika kwa siku 12 ambapo siku 6 za mwanzo ni uandaaji wa  Mpango Mkakati wa Wizara na kuanzia siku ya 7 hadi 12 ni uandaaji wa Mpango wa ufuatiliaji wa Mpango huo, na kusisitiza kufanya kazi kwa bidii na ufanisi kwasababu kila siku ina kipengele cha kufanyia kazi.

 

Kwa upande wa Jane Kaji mwezeshaji kutoka Ofisi Ya Rais Utumishi na Utawala Bora amesema kuwa Mpango Mkakati wa Utendaji Kazi na Ufuatiliaji ni mfumo wa Utendaji kazi ambao unatoa mwongozo kwa watumishi wa umma katika kutoa huduma bora kwa jamii, uwazi na uwajibikaji.