Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

TEKNOLOJIA ZA KIDIJITALI KUONGEZA UFANISI WA HUDUMA ZA POSTA NA BIASHARA MTANDAO


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), amesema matumizi ya teknolojia za kisasa, zikiwemo Akili Unde (AI), Mtandao wa Vitu (IoT), uchambuzi wa data, Mfumo wa Kitaifa wa Anwani za Makazi (NaPA) na mifumo ya ufuatiliaji wa vifurushi kwa wakati halisi, yana mchango mkubwa katika kuboresha huduma za posta, usafirishaji wa barua, vipeto, vifurushi, mizigo na kukuza biashara mtandao.

Dkt. Mkama ameyasema hayo tarehe 14 Oktoba 2026 jijini Arusha, wakati akifungua rasmi Jukwaa la 5 la Mwaka la Jumuiya ya Mawasiliano ya Afrika Mashariki (EACO) kuhusu Posta na Usafirishaji (EPLF 5).

Amesema jukwaa hilo ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa Kikanda, kubadilishana uzoefu na kuendeleza Sekta ya Posta na Usafirishaji ili iendane na mahitaji ya uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali, miundombinu ya pamoja na mifumo inayowasiliana ili kupunguza vikwazo vya biashara za mipakani, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Akizungumzia Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA), Dkt. Mkama amesema matumizi ya anwani sahihi ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuboresha mipango ya ugavi na kupanua upatikanaji wa huduma za kidijitali. 

Ameongeza kuwa mitandao ya posta inapaswa kutumika kuwaunganisha wazalishaji na masoko, pamoja na kuwawezesha wajasiriamali, hususan vijana na wakazi wa maeneo ya vijijini, kunufaika na fursa za biashara mtandao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mkama amezitaka nchi wanachama wa EACO kushiriki kikamilifu katika maonesho ya jukwaa hilo kwa kuwasilisha ubunifu, teknolojia na mafanikio yao katika Sekta ya Posta na Usafirishaji.

Jukwaa la EPLF 5 linafanyika kuanzia 14 hadi 16 Oktoba, 2026 huku likiongozwa na kaulimbiu isemayo “Driving Regional Integration, Smart Innovation and Sustainable Trade in East Africa,” inayosisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa Kikanda, kuendeleza ubunifu na kukuza biashara endelevu katika nchi za Afrika Mashariki.